Afrika imeelezea nia yake ya kupanua ushirikiano na maendeleo na nchi za Amerika Kusini na Karibia.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026, ambae ni Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye Jumamosi katika Mkutano wa 10 wa Jumuiya ya Mataifa ya Amerika Kusini na Karibi CELAC, uliofanyika Bogota, Colombia.
Mwaka huu Columbia iliandaa mkutano wa kilele wa CELAC-Africa 2026.
Rais Ndayishimiye kwa mujibu wa ofisi yake “ameangazia uwezo kati ya uchumi wa Afrika na ule wa CELAC, hasa katika kilimo, nishati na viwanda.”
Amesisitiza kuwa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika, AfCFTA, mpango wa kukuza biashara ya ndani ya Afrika, ni njia ya uwekezaji huu.
“Manufaa ya AfCFTA ni kuwa ushirikiano unaweza kutafsiri katika fursa halisi za uwekezaji na thamani ya kikanda,” Rais Ndayishimiye aliuambia mkutano wa marais uliohudhuriwa na wawakilishi wa nchi 33.
Rais wa Colombia Gustavo Petro, anayemaliza muda wake wa zamu kama rais wa Jumuiya ya Amerika ya Kusini na Karibia alisisitiza kuwa kufunguka kwa mipaka kumefungua fursa kote ulimwenguni.
“Tunaamini utamaduni ni wa heshima, na kama Watu wa Amerika ya Kusini, tunakubali hili. Suala si kugombana kwa watu wa tamaduni na sera tofauti bali kuanzisha mazungumzo kati yao,” alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo.
Pia alisisitiza haja ya ushirikiano zaidi na hatua za pamoja ili kukabiliana na changamoto za kimataifa kama vile mgogoro wa mabadiliko ya hali ya hewa, akionya kwamba binadamu wanakabiliwa na ongezeko la ukosefu wa utulivu na hatari za kimataifa.
Akiangazia uwezo wa Marekani ya Kusini wa kukuza nishati safi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, Rais Petro alisisitiza jukumu muhimu la kanda katika kutatua matatizo ya kimataifa.
Huku akikiri kuwa kuna tofauti nyingi kati ya nchi duniani, Rais alisisitiza kuwa umoja mpya lazima ujengwe kupitia mazungumzo ya wazi na ya kweli kati ya watu tofauti.
Columbia imekabidhi urais wa zamu wa shirika hilo kwa Uruguay chini ya Rais Yamandu Orsi.














