Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, pamoja na Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (MIT) Ibrahim Kalın, wamekutana jijini Ankara na Rustem Umerov, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa na Ulinzi la Ukraine. Mkutano huo umeashiria mwanzo wa shughuli za kidiplomasia za Uturuki katika mwaka mpya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, mazungumzo hayo yalifanyika Alhamisi, bila kutolewa maelezo ya kina kuhusu yaliyojadiliwa. Hata hivyo, mkutano huo umefanyika wakati ambapo matumaini ya kimataifa yanaongezeka juu ya uwezekano wa juhudi mpya za kidiplomasia kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine, vinavyokaribia kuingia mwaka wa nne.
Vyanzo vya usalama vimeeleza kuwa Umerov na Kalın walijadili hali ya usalama nchini Ukraine, maendeleo ya mzozo na athari zake za kikanda na kimataifa. Mazungumzo hayo pia yalihusu juhudi za kufikia suluhu ya amani na suala la kubadilishana wafungwa wa kivita.
Uturuki, inayodumisha uhusiano wa kikazi na Moscow na Kiev, imeendelea kujipambanua kama mpatanishi muhimu katika mzozo huo, ikiimarisha nafasi yake katika juhudi za kidiplomasia za kikanda na kimataifa.
CHANZO: TRT Afrika














