Afrika

Baraza la Makanisa nchini Kenya lajitenga na mhubiri anayedai miujiza ‘Nabii Owour’

Mhubiri David Owuor amezua mjadala mkali kufuatia madai yake ya kuwa na uwezo wa kutibu maradhi kama ukimwi na saratani na kutabiri majanga makubwa

Newstimehub

Newstimehub

6 Januari, 2026

a201ec6c1807caaa83970ebe75dbe9661d68f6042f64c6c7ef5314f23e50baf4

Mvutano mpya umeibuka nchini Kenya kati ya Baraza la Makanisa NCCK na mhubiri maarufu anayejiita nabii, David Owuor.

Baraza hilo la Makanisa limetoa tangazo kujitenga na madai ya Owour kuwa ana uwezo wa kuponya maradhi kimiujiza na pia limewatahadharisha waumini kutofuata kama upepo wahubiri wanaotoa madai kama hayo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Baraza lilisema haliungi mkono wala kuhimiza matamko yanayodai kuwa wachungaji au manabii binafsi wana uwezo wa kuponya magonjwa.

NCCK walieleza kuwa uponyaji ni suala la Mwenyezi Mungu na halifai kuwasilishwa kama ni uwezo binafsi wa kiongozi yeyote wa dini.

Uponyaji wa Ukimwi

Hii inafuatia madai ya mhubiri Owuor Januari mosi kuwa ameweza kuwaponya mamia ya watu waliokuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi, walio na saratani au ulemavu.

Mhubiri huyo alichapisha pia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X nyaraka za uchunguzi wa damu kutoka kwa watu wanaodai kuponywa kwa miujiza ya mhubiri huyo.

Lakini katika taarifa yao Baraza la Makanisa la Kenya lilionya kwamba madai ya umma ya uponyaji yanaweza kuwapotosha waumini, haswa wale ambao ni wagonjwa na waliokata tamaa ya tumaini.

Pia walisema matamshi kama hayo yanaweza kuwasukuma watu kuacha matibabu, na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Vyombo vya serikali viingilie kati

Sasa Baraza hilo limetoa wito kwa vyombo vya dola na maafisa wa afya kusaidia kuwalinda wananchi dhidi ya taarifa potofu za kiafya na kuhimiza ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa dini na wataalam wa matibabu ili kulinda afya ya umma.

Upande wa serikali, kulikuwa na kauli kali zaidi ambapo Waziri wa Afya Aden Duale alitaka uchunguzi kuanzishwa dhidi ya mhubiri huyo na ikiwezekana afunguliwe mashtaka.

Wakenya mtandaoni wamekuwa na kauli za kutofautiana huku baadhi wakiunga mkono amri ya kukamatwa na kushtakiwa kwa Owuor na wenzake. Lakini wapo wanaomtetea na kusema kuwa Owuor kwamba anao uwezo wa kuwaponya wagonjwa.

Haya yanawakumbusha Wakenya matukio ya 2023 ya Shakahola, ambapo zaidi ya watu 400 walifariki kutokana na kumfuata mhubiri wa kanisa la Good News International, Paul Mackenzie, aliyewaagiza kufunga kula na kunywa ili waende kukutana na Yesu Kristu.

Owuor alianzaia wapi?

Mhubiri huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mauaji, ugaidi, utesaji watoto na mauaji bila kukusudia. Kesi yake bado inaendelea.

Mhubiri Owuor anaongoza kanisa la Repentance and Holiness. Anaaminiwa kumiliki shahada ya uzamivu katika biokemia na alifanya kazi kama mhadhiri wa chuo nchini Marekani kabla ya kurudi Kenya mwaka 2000 na kuanzisha kanisa lake.

Owuor, mbali na madai yake ya kutibu kwa kutumia miujiza, lakini pia amezua mjadala mkubwa kutokana na madai yake ya kuwa na uwezo wa kutabiri majanga makubwa ya dunia kabla hayajatokea.

Pia ni miongoni mwa wahubiri matajiri zaidi nchini Kenya akidaiwa kumiliki magari ya kifahari, ndege za binafsi na majumba makubwa ya yakifahari, huku akionekana katikati ya walinzi akiwa katika msafara mrefu kila anapokwenda.