Angalau wanajeshi 8 wa Nigeria wameuawa na wengine 50 kujeruhiwa baada ya magaidi wa Boko Haram kushambulia kikosi cha kijeshi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu, ambapo magaidi walifika kwa pikipiki na magari ya kivita na kuanzisha mapigano makali.
Jeshi la Nigeria lilisema kikosi hicho kilikuwa sehemu ya operesheni ya kusafisha magaidi katika eneo la Timbuktu Triangle. Baada ya mapigano, jeshi lilitangaza kuwa limefanikiwa kuondoa magaidi na kuvuruga mashambulizi yaliyopangwa kwa kutumia magari yenye mabomu. Hata hivyo, gari moja lililokuwa na mabomu liliweza kupenya ngome za ulinzi na kuua wanajeshi kadhaa pamoja na wanachama wa Civilian Joint Task Force (CJTF).
Boko Haram, kundi la kigaidi lililoibuka mwaka 2009, limeua maelfu na kusababisha mamilioni kuyahama makazi yao nchini Nigeria na mataifa jirani. Jeshi limehamisha vikosi vyake kutoka Timbuktu Triangle hadi kambi ya Damboa, huku majeruhi na miili ya waliouawa ikipelekwa hospitali ya kijeshi Maimalari Barracks, Maiduguri.
CHANZO: TRT Afrika














