Bunge la Taifa la Algeria (APN) limeidhinisha rasmi muswada wa sheria unaotangaza ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuwa ni uhalifu wa kiserikali. Sheria hiyo ilipitishwa kwa kauli moja katika kikao cha bunge kilichofanyika Jumatano, Desemba 24, kwa ushiriki wa wabunge wote.
Muswada huo, unaojumuisha zaidi ya vifungu 30, umejengwa juu ya misingi ya sheria za kimataifa pamoja na Katiba ya Algeria, ambayo inalinda haki ya mataifa kujitawala na kudai haki ya kihistoria. Lengo kuu la sheria hiyo ni kuhalalisha kisheria uhalifu wa ukoloni wa Ufaransa kuanzia uvamizi wa Juni 14, 1830 hadi uhuru wa Algeria Julai 5, 1962, pamoja na athari zake zote kwa wananchi wa Algeria.
Baada ya mjadala wa siku kadhaa, muswada huo ulifanyiwa marekebisho kadhaa, ambapo vitendo kama mauaji ya raia, mateso, matumizi ya silaha zilizopigwa marufuku, mashambulizi ya kijeshi na sheria za kibaguzi dhidi ya wazawa viliorodheshwa rasmi miongoni mwa uhalifu wa kikoloni.
Kwa mujibu wa toleo la mwisho la sheria hiyo, ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria umetajwa kuwa “uhalifu wa dola unaokiuka misingi na maadili ya kibinadamu, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni yaliyotambuliwa na sheria na mikataba ya kitaifa na kimataifa.” Sheria hiyo pia inaelekeza serikali ya Algeria kukusanya, kuhifadhi na kusambaza ukweli wa kihistoria kuhusu kipindi cha ukoloni.
Sheria hiyo imetaja aina 27 za uhalifu wa kikoloni, zikiwemo mauaji ya raia, mashambulizi ya kijeshi dhidi ya watu wasio na silaha, matumizi ya nguvu kupita kiasi, silaha zisizoruhusiwa kimataifa, mabomu ya nyuklia, ulipuaji wa mabomu ya majaribio, kunyonga bila hukumu, uporaji wa mali za umma, utekelezaji wa sheria za dharura kwa Waalkeria pekee, pamoja na mateso ya kimwili na kisaikolojia.
Kwa mujibu wa historia, wazo la kuunda sheria dhidi ya uhalifu wa kikoloni lilianza kujadiliwa tangu mwaka 1984, lakini lilikumbwa na vikwazo vingi. Majaribio mengine yalifanyika tena mwaka 2001, 2005, 2006, 2017, 2020 na 2021, bila mafanikio hadi sasa.
Mwisho wa Novemba mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf, alitoa wito wa kuhalalishwa kwa uhalifu wa ukoloni barani Afrika, akieleza kuwa ukoloni ulihusisha mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa asili pamoja na uporaji wa rasilimali zao. Alisisitiza kuwa ni wakati wa kulaani ukoloni kwa ujumla wake, badala ya kuangazia athari zake chache pekee.
Kwa mujibu wa Attaf, Afrika ina haki ya kudai kutambuliwa rasmi kwa uhalifu uliofanywa dhidi ya watu wake wakati wa ukoloni, pamoja na kudai fidia na kurejeshwa kwa mali zilizoporwa.
Kupitishwa kwa sheria hiyo kunakuja wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya Algeria na Ufaransa ukiwa katika hali mbaya, hali iliyozidishwa na mvutano wa kisiasa unaoendelea tangu majira ya joto ya mwaka 2024. Migogoro ya kihistoria imeendelea kuwa chanzo kikuu cha msuguano, huku Algeria ikiendelea kudai Ufaransa itambue rasmi uhalifu wa kikoloni—madai ambayo hadi sasa hayajapatiwa majibu chanya kutoka Paris.
CHANZO: AA














