Burkina Faso na Mali zimetangaza kuanza kutekeleza vikwazo vya viza kwa raia wa Marekani kama hatua ya kulipiza kisasi, kufuatia uamuzi wa Washington kuongeza marufuku ya usafiri kwa mataifa kadhaa, hususan barani Afrika.
Hatua ya Burkina Faso imekuja baada ya nchi hiyo kuorodheshwa kwenye marufuku kamili ya kusafiri kwenda Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump. Wizara ya Mambo ya Nje ya Burkina Faso ilisema kuwa nchi hiyo itaweka masharti sawa ya viza kwa raia wa Marekani, ikisisitiza kuwa uamuzi huo umezingatia kanuni ya uwiano katika mahusiano ya kimataifa.
Katika taarifa yake, serikali ya Ouagadougou ilibainisha dhamira yake ya kuheshimu usawa wa mataifa huru na kuendelea kushirikiana na washirika wote kwa misingi ya kuheshimiana na maslahi ya pande zote.
Nayo Mali, pamoja na Niger, imechukua msimamo kama huo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali ilitangaza kuwa, kuanzia mara moja, raia wa Marekani watahitajika kutimiza masharti yale yale ya viza yanayotumika kwa raia wa Mali wanaoingia Marekani, kwa kuzingatia kanuni hiyo hiyo ya uwiano.
Awali, Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametangaza vikwazo vipya vya usafiri vinavyohusisha marufuku kamili au ya sehemu kwa takribani nchi 39, nyingi zikiwa barani Afrika. Marufuku hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi tarehe 1 Januari 2026, na inalenga kuzuia au kupunguza uingiaji wa raia wa mataifa husika nchini Marekani.
CHANZO: TRT Afrika














