Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, Elon Musk, ameweka rekodi mpya ya utajiri baada ya thamani ya mali yake kufikia takriban dola za Marekani bilioni 749, na hivyo kuwa mtu wa kwanza duniani kuvuka kiwango cha dola bilioni 700. Haya yanatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Delaware kurejesha kifurushi cha hisa za Tesla chenye thamani ya dola bilioni 139, ambacho kilikuwa kimefutwa mwaka uliopita.
Kifurushi hicho cha malipo kilitokana na mpango wa mwaka 2018, ambao awali ulikadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 56. Mwaka 2024, mahakama ya chini ilikuwa imekifuta, ikikieleza kuwa hakikuwa sahihi na hakikuwa cha haki. Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Delaware ilibatilisha uamuzi huo Ijumaa, ikisema kuwa kufutwa kwa kifurushi hicho hakukuwa sahihi na kulimkosea haki Musk.
Mapema wiki hii, Musk pia aliingia kwenye historia kwa kuwa mtu wa kwanza duniani kuvuka utajiri wa dola bilioni 600, baada ya taarifa kuibuka kwamba kampuni yake ya anga, SpaceX, huenda ikaingia sokoni kwa kuuza hisa zake kwa umma, hatua iliyoongeza thamani ya mali yake kwa kiasi kikubwa.
Aidha, mwezi Novemba, wanahisa wa Tesla waliidhinisha mpango mwingine mkubwa wa malipo kwa Musk unaokadiriwa kufikia dola trilioni moja, ukiwa ndio mpango mkubwa zaidi wa aina hiyo katika historia ya makampuni. Wawekezaji walisema wanaunga mkono maono ya Musk ya kuigeuza Tesla kutoka kampuni ya magari ya umeme pekee hadi kuwa kinara katika teknolojia ya akili bandia na roboti.
Kwa mujibu wa orodha ya bilionea ya Forbes, utajiri wa Musk sasa unamuweka mbali sana na mtu wa pili tajiri zaidi duniani, Larry Page, mwanzilishi mwenza wa Google, kwa tofauti ya takriban dola bilioni 500.
CHANZO: TRT Afrika














