Serikali ya Ghana imempa uraia mtengeneza maudhui ya YouTube kutoka Marekani, Darren Jason Watkins Jr. maarufu kama IShowSpeed. Waziri wa Mambo ya Nje Sam Okudzeto Ablakwa alitangaza uamuzi huo kupitia mtandao wa X, akisema serikali imeidhinisha kumpa pasi ya kusafiria ya Ghana baada ya kuthibitisha uhusiano wake wa dhati na taifa hilo.
IShowSpeed, kijana mwenye umri wa miaka 21 aliyezaliwa Cincinnati, Ohio, ni mmoja wa watengeneza maudhui wenye ushawishi mkubwa mtandaoni. Katika ziara yake ya mwezi mmoja barani Afrika, alifikia jumla ya wafuasi milioni 50 kwenye YouTube, huku Forbes ikikadiria thamani yake kuwa dola milioni 20.
Ziara yake, iliyoanza Desemba 29, ilimfikisha katika nchi 20, ikiwemo Botswana, Ethiopia na Morocco, ambapo alionyesha mamilioni ya mashabiki wake taswira tofauti ya Afrika kupitia migodi ya almasi, vyakula vya kienyeji na mashindano ya AFCON.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wamesema IShowSpeed ameonesha Afrika kwa sura mpya na chanya, tofauti na taswira hasi mara nyingi inayoonekana kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.
CHANZO: TRT Afrika














