Kampeni ya kimataifa imenzishwa upya Jumatatu ikitaka kuachiwa kwa kiongozi wa Kipalestina, Marwan Barghouti, ambaye amekuwa akikabili kifungo cha maisha mara tano nchini Israel tangu 2002 kutokana na mashtaka ya kipindi cha Intifada ya Pili. Barghouti, mwenye umri wa miaka 66 na mwanachama mwandamizi wa Fatah, anachukuliwa kuwa mmoja wa viongozi muhimu zaidi katika siasa za Palestina. Kampeni hiyo imezinduliwa kupitia matukio ya wakati mmoja London, Afrika Kusini, Ufaransa, Italia, nchi za Kiarabu, na katika kijiji chake cha Kobar, Ukingo wa Magharibi. Waandaaji, wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu na washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, wanasisitiza haja ya kuharakisha juhudi za kuwaachia wafungwa wa Kipalestina, huku zaidi ya watu 90 wakiripotiwa kufariki gerezani Israel tangu Oktoba 2023. Barghouti, anayechukuliwa kuwa kiongozi pekee anayeweza kuunganisha makundi yote ya kisiasa ya Palestina, hakujumuishwa katika orodha ya wafungwa waliotakiwa kuachiwa chini ya makubaliano ya kusitisha vita yaliyotekelezwa Gaza tarehe 10 Oktoba. Makubaliano hayo, ambayo yalisitisha vita vya miaka miwili vilivyoua zaidi ya watu 70,000 na kujeruhi zaidi ya 171,000 wengi wao wanawake na watoto, yanajumuisha kubadilishana mateka na wafungwa, kujenga upya Gaza na kuanzisha utawala mpya bila Hamas.
“Kumuachia Marwan”: Kampeni ya Kimataifa Yadai Kuachiwa kwa Kiongozi wa Kipalestina
Matukio yaliyofanyika kwa wakati mmoja katika nchi kadhaa, zikiwemo Uingereza na Ufaransa, yanataka kuachiwa kwa Marwan Barghouti, ambaye amekuwa gerezani Israel tangu 2002.














