Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi (UNHCR) linasema karibu watu 100,000 wamekimbia makazi yao katika kipindi cha wiki mbili kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji. Visa vya vurugu sasa vinaingia katika wilaya ambazo hapo awali zilikuwa salama, na maelfu wakikimbia usiku huku vijiji vikichomwa moto na raia kushambuliwa.
UNHCR inaonya kuwa mahitaji ya dharura yanazidi uwezo wa mashirika ya misaada, huku familia zikikimbia mara ya pili au ya tatu mwaka huu. Tangu 2017, mgogoro huo umeathiri zaidi ya watu milioni 1.3, lakini mwaka 2025 umeleta ongezeko jipya la mashambulizi hadi mkoa wa Nampula. Wanawake, wasichana na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za unyanyasaji na matatizo ya kiafya huku wengi wakiwasili wakiwa wamechoka, wamedhoofu na bila hati muhimu za utambulisho.













