Waasi wametekeleza shambulio la kikatili katika kijiji cha Guidado, eneo la Kaskazini Magharibi mwa Cameroon, na kuua watu 14, wakiwemo watoto saba wenye umri wa kati ya miaka miwili hadi kumi na moja. Tukio hilo liliripotiwa na televisheni ya taifa CRTV, likieleza kuwa miongoni mwa waliouawa ni wanawake sita na mwanaume mmoja.
Gavana wa eneo hilo, Adolphe Lele Lafrique, alisema kuwa manusura 14 wamepelekwa hospitali jirani kwa matibabu, huku Rais Paul Biya akiamuru hatua za haraka kurejesha usalama na amani.
Mashambulizi ya aina hii yamekuwa ya mara kwa mara katika maeneo ya Kianglophone, ambapo makundi ya waasi wanaotaka kujitenga huwalenga raia, viongozi wa mitaa, walimu na maafisa wa serikali kwa madai ya kushirikiana na mamlaka ya taifa. Serikali ya Cameroon imesisitiza tena kuwa nchi hiyo itaendelea kubaki kama dola moja lenye umoja.
CHANZO: TRT Afrika














