Watu kadhaa wamepoteza maisha kufuatia mlipuko uliotokea ndani ya msikiti wakati wa sala ya jioni siku ya Jumatano katika eneo la Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno kaskazini-mashariki mwa Nigeria, kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo.
Vyanzo vya eneo hilo vimesema kuwa mlipuko huo ulitokea wakati wa waumini wakiwa wamekusanyika kwa ibada, hali iliyosababisha vifo na majeruhi. Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa takriban watu saba waliuawa katika tukio hilo, ingawa idadi kamili ya waathirika bado inathibitishwa na mamlaka.
Jimbo la Borno limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye msimamo mkali, hali iliyosababisha vifo vya maelfu ya raia na kuwalazimu mamilioni ya watu kuyahama makazi yao katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Hadi sasa, hakuna kundi lililojitokeza kudai kuhusika na shambulio hilo la Jumatano. Hata hivyo, katika matukio ya awali, makundi ya kigaidi yamekuwa yakilenga misikiti na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu mjini Maiduguri, kwa kutumia mashambulizi ya kujitoa mhanga au vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji.
Kundi la Boko Haram lilianza mashambulizi yake katika jimbo la Borno mwaka 2009, na tangu wakati huo limekuwa tishio kubwa kwa usalama wa eneo hilo. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Nigeria imeongeza juhudi za kijeshi na kiusalama ili kudhibiti na kudhoofisha shughuli za kundi hilo.
CHANZO: TRT Afrika














