Rais Yoweri Museveni aliliambia taifa Jumapili kuwa ushindi wake mkubwa katika uchaguzi wa Uganda wa Januari 15 ulionyesha udhibiti wa chama chake.
Museveni alisema siku moja baada ya kutangazwa mshindi kwamba matokeo yalitoa “taswira nzuri ya nguvu” ya chama chake, cha National Resistance Movement maarufu NRM.
“Upinzani una bahati,” alisema kuhusu ushindi wake baada ya idadi ndogo ya wapiga kura kujitokeza katika uchaguzi wa Alhamisi. “Bado hawajaona nguvu yetu kamili.”
Uwiano wa wapiga kura ulikuwa asilimia 52, kiwango cha chini tangu Uganda irudi katika mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 2006.
Bobi Wine ana chaguo la kwenda mahakamani
Akihutubia taifa kutoka nyumbani kwake magharibi mwa Uganda, ambapo wageni wengi walikusanyika kumpongeza, Rais Museveni alihutubia hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa mshindi kwa asilimia 71.6. Museveni alisema kuwa anaamini wengi ambao hawakupiga kura walikuwa wanachama wa NRM.
Mpinzani wa karibu Museveni na kiongozi wa upinzani wa Uganda, Bobi Wine, alipata asilimia 24.7 ya kura.
Wine, mwenye umri wa 43, mwanamuziki ambae baadae alikuwa mwanasiasa jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, ambae amedai matokeo hayo ni batili ana chaguo la kuwasilisha madai yake ya kupinga matokeo mahakamani.
Huu utakuwa ni muhula wa saba wa Rais Museveni tangu kuingia madarakani. Wafuasi wake wanaomuona kuwa ndiye aliyeleta amani na utulivu nchini humo. Uganda kwa miongo kadhaa imekuwa makazi ya maelfu ya wakimbizi kutoka maeneo mengine ya eneo hilo.
Kuzimwa kwa intaneti
Katika hotuba yake Jumapili, Museveni aliutuhumu upinzani kwa kujaribu kuchochea machafuko wakati wa upigaji kura. Aliwaomba viongozi wa dini kuwafikia vijana ambao wanaweza kupotoshwa na kuingia kwenye ghasia.
Uchaguzi wa Uganda uliathiriwa na kuzimwa kwa huduma ya intaneti kwa siku kadhaa na kushindwa kufanya kazi kwa baadhi ya mashine za kupigia kura kwa njia ya biometriki, jambo lililosababisha kuchelewa kuanza kwa upigaji kura katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na Kampala, mji mkuu.
Bobi Wine pia amedai kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika maeneo kadhaa yanayochukuliwa kuwa ngome za Museveni, lakini serikali inakanusha madai hayo.














