Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), unaojumuisha Mali, Burkina Faso na Niger, umeanzisha kituo kipya cha televisheni chenye lengo la kupambana na upotoshaji wa taarifa na kuimarisha mawasiliano ndani ya kanda hiyo ya Afrika Magharibi.
Kituo hicho, kinachojulikana kama Televisheni ya AES, kimewekwa rasmi kama chombo cha habari cha muungano huo na kinatarajiwa kutoa taarifa zinazolenga kuwasilisha mtazamo wa pamoja wa nchi wanachama, sambamba na kukabiliana na kile kinachoelezwa kuwa ni simulizi potofu kuhusu eneo la Sahel.
Uzinduzi wa televisheni hiyo ulifanyika Jumanne mjini Bamako, Mali, wakati wa mkutano wa siku mbili wa viongozi wa muungano huo. Hafla hiyo iliongozwa na Rais wa Mali Jenerali Assimi Goita, Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traore na Rais wa Niger Jenerali Abdourahamane Tiani, waliokutana kutathmini mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa AES.
Hatua hii inakuja baada ya Mali, Burkina Faso na Niger kujiondoa rasmi katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) mwezi Januari 2025, kufuatia mchakato wa majadiliano uliochukua karibu mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais wa Burkina Faso, mkutano huo wa Bamako uliwaleta viongozi pamoja ili kupitia utekelezaji wa maamuzi ya awali, kubainisha mafanikio yaliyopatikana na kutafuta suluhu kwa changamoto zinazoikabili AES. Rais Traore pia alipanga kukutana na raia wa Burkina Faso wanaoishi nchini Mali.

Mbali na uzinduzi wa kituo cha televisheni, muungano huo umechukua hatua nyingine za kuimarisha mshikamano wake, ikiwemo kuanzishwa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi cha AES (FU-AES) chenye makao yake makuu mjini Niamey. Kikosi hicho kinatarajiwa kuwa na takribani wanajeshi 5,000 kwa ajili ya kupambana na makundi yenye silaha katika eneo la Sahel.
Aidha, AES imeanzisha Benki ya Uwekezaji na Maendeleo ya AES (BCID-AES) yenye mtaji wa awali wa faranga za CFA bilioni 500, sawa na karibu dola milioni 900 za Marekani, kwa lengo la kufadhili miradi ya miundombinu, nishati na kilimo bila kutegemea misaada ya nje.
Kwa jumla ya idadi ya watu inayokadiriwa kufikia milioni 78, muungano wa AES unaendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja za usalama, uchumi na mawasiliano, ukiashiria mwelekeo wa kujitegemea zaidi katika eneo la Sahel.
CHANZO: TRT Afrika














