Afrika

Mwalimu Mkenya aripotiwa kuuwawa Tanzania

John Okoth Ogutu, Mkenya mwenye umri wa miaka 33 aliyeishi Tanzania kwa zaidi ya miaka kumi, ameripotiwa kuuawa kwa risasi wakati wa machafuko yaliyotokea Dar es Salaam baada ya uchaguzi.

Newstimehub

Newstimehub

5 Novemba, 2025

e3b0be332ad039c7d69110a728ee9a0ff2c7e8a9359477b9300da645da0035ad

Kwa mujibu wa familia yake, waliarifiwa kuwa Ogutu, aliyekuwa akifundisha katika Shule ya Msingi ya Sky School, alipigwa risasi jijini Dar es Salaam wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 29.

Aidha mwili wake unaripotiwa kuhifadhiwa katika hospitali moja jijini humo na familia yake iko mbioni kupata taarifa zaidi kuhusu sehemu mwili ulipo.

“Vita vimenza tukapata habari kwamba amepigwa risasi,” Jennifer Otieno, dada yake John Okoth Ogutu amesema.

Naye kaka yake Benard Brian ameongeza ya kuwa: “Tumepatwa na huzuni sana. Kwa wale Wakenya walienda kibiashara, hivi sasa taarifa ambazo tunapata ni kwamba Wakenya wanadhulumiwa. Wakenya wamewekwa kama wahalifu. Ndugu yetu hakuwa mhalifu.”

Licha ya juhudi za kutafuta taarifa, ikiwemo kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya na kufika Ubalozi wa Tanzania, familia imesema haijapokea maelezo yoyote kuhusu mipango ya kurejesha mwili au hali ya Wakenya wengine waliokumbwa na vurugu hizo.