Katibu Mkuu wa chama cha National Democratic Congress (NDC), Mambwe Zimba, ameripotiwa kukamatwa mjini Lusaka kwa tuhuma za kusambaza picha iliyohaririwa mtandaoni inayomuonesha Rais Hakainde Hichilema akiwa ndani ya jeneza.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya nchini humo, kitengo cha uhalifu wa mitandaoni kilianza uchunguzi baada ya kupokea malalamiko kuhusu ukurasa wa Facebook unaoitwa “Zambia kwa Wote 2026.” Uchunguzi ulisababisha kukamatwa kwa Zimba mwenye umri wa miaka 44 pamoja na kukamatwa kwa simu inayodaiwa kuhusika na tukio hilo.
Polisi wamesema picha hiyo ilikuwa ya kupotosha na ingeweza kuzua taharuki kwa umma. Zimba kwa sasa anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Lusaka huku uchunguzi ukiendelea, na mamlaka zikisema huenda watu wengine wakaingizwa katika kesi hiyo.
CHANZO: TRT Afrika














