Rais wa Ghana, John Mahama, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuunga mkono azimio la kutambua rasmi madhila ya kihistoria yaliyosababishwa na biashara ya utumwa wa Atlantiki. Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa AU mjini Addis Ababa, Mahama alisema kuwa ingawa hatua hiyo haiwezi kufuta yaliyopita, itakuwa ni kukiri kwamba utumwa wa Waafrika na utumwa wa kikabila ulikuwa uhalifu mkubwa ulioshiriki katika kujenga dunia ya kisasa.
Mahama alisisitiza kuwa kukabiliana na ukweli wa kihistoria ni tendo la “uthubutu wa kimaadili” na si chanzo cha mgawanyiko. Aliongeza kuwa athari za utumwa bado zinaonekana leo kupitia ukosefu wa usawa wa kimuundo, ubaguzi wa rangi na pengo la kiuchumi.
Kwa mujibu wake, kupitishwa kwa azimio hilo kutakuwa mwanzo wa mchakato wa mazungumzo ya kudumu kuhusu haki ya marekebisho na uponyaji wa kijamii. Ghana, alisema, itaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Tume ya AU na nchi wanachama husika ili kuendeleza mchakato huo.
CHANZO: AA














