Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TİKA) limeanzisha mpango wa maendeleo ya kijamii nchini Msumbiji wenye lengo la kuwasaidia wanawake waliopitia vurugu na dhulma za kingono, ili waweze kurejea katika maisha ya kawaida ya kijamii na kiuchumi.
Mradi huo unawalenga wanawake walionusurika matukio ya ukatili, ukiwa na lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuwapa ujuzi wa kujitegemea. Wanufaika wa mpango huo wameunganishwa chini ya Shirikisho la Hixikanwe, ambalo linahusika na shughuli za kuwawezesha wanawake katika jamii.
Kama sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, TİKA imeweka jiko la kisasa litakalotumika kama kituo cha mafunzo ya kitaalamu kwa wanawake hao, huku pia likiwawezesha kujipatia kipato kupitia shughuli za uzalishaji wa chakula.

Aidha, mradi huo unajumuisha ujenzi wa kizimba maalumu cha kuuza vyakula, ambacho kitawawezesha wanawake kutangaza na kuuza bidhaa wanazotengeneza, na hivyo kupata chanzo endelevu cha mapato.
Kupitia mpango huu, TİKA inalenga kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa wanawake walionusurika vurugu, kuwasaidia kujenga upya maisha yao, na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla nchini Msumbiji.
CHANZO: TRT Afrika














