Afrika

Simba Sports Club ya Tanzania ‘yamtimua’ Dimitar Pantev

Pantev alichukua mikoba ya kuwafundisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ mwezi Oktoba 2025, akitokea Gaborone United ya Botswana.

Newstimehub

Newstimehub

2 Desemba, 2025

22c5e6d55231dc25a8c3df87bff09c2ab4f8c16c718401980e8bf3ae4f71fbfa

Klabu ya soka ya Tanzania, Simba imesitisha mkataba na aliyekuwa meneja mkuu Dimitar Pantev pamoja na wasaidizi wake wawili.

Kulingana kwa taarifa ya umma iliyotolewa na Simba Sports Club kupitia ukurasa wake wa X (zamani twitter), Simba imefikia makubaliano hayo ya pande mbili, huku kikosi hicho sasa kikiwa chini ya kocha Selemani Matola, wakati mchakato wa kutafuta kocha mwingine ukiendelea.

Uamuzi  huo unakuja siku mbili baada ya Simba Sports Club kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Stade Malien ya Mali, katika mchezo Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika, uliofanyika Novemba 30 mjini Bamako.

Kabla ya hapo, timu hiyo ilipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Petro de Luanda ya nchini Angola.

Pantev alichukua mikoba ya kuwafundisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ mwezi Oktoba 2025, akitokea Gaborone United ya Botswana.

Raia huyo wa Bulgaria alirithi mikoba iliyoachwa wazi na Fadlu davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco.