Tanzania, Zambia na China zimetiliana saini mkataba wa Dola Bilioni 1.4, kwa lengo la kufufua reli ya TAZARA.
Mkataba huo, utahusisha ukarabati wa njia ya reli yenye urefu wa kilomita 1,860, ununuzi wa vichwa 34 vya treni, na mabehewa 16 ya abiria.
Mkataba huo, ambao ulihusisha miezi 18 ya majadiliano, utahusisha ukarabati wa karakana kwa ajili ya reli hiyo yenye kuunganisha jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania hadi Kapiri Mposhi, Zambia.
“Ufufuaji wa huduma hii utagharimu uwekezaji wa awali wa Dola Bilioni 1.1na kiasi kingine kitakachogharimu Dola Milioni 238,” alisema Ernest Chanda, msemaji wa Wizara ya Usafirishaji ya Zambia, katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumatatu, jijini Lusaka.
Reli ya TAZARA ilianzishwa mwaka 1976, kama alama ya mshikamano kati ya Tanzania na Zambia, kwa msaada wa serikali ya China.
Kwa miaka mingi, reli ya TAZARA imekuwa kiungo muhimu cha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi.














