Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani inaweza kufanya mashambulizi mengine ya anga nchini Nigeria endapo mauaji ya Wakristo yataendelea. Kauli hiyo aliitoa katika mahojiano na gazeti la The New York Times, akizungumzia shambulizi la anga lililofanywa na Marekani siku ya Krismasi dhidi ya wanamgambo wa Daesh kaskazini-magharibi mwa Nigeria.
Trump alisema angependa shambulizi hilo liwe la mara moja, lakini akaonya kuwa endapo mauaji ya Wakristo yataendelea, mashambulizi yanaweza kurudiwa. Alikiri kuwa pia Waislamu wanauawa nchini Nigeria, lakini akadai kuwa Wakristo ndio wanaolengwa zaidi.
Kwa upande wake, serikali ya Nigeria imekanusha vikali madai ya mateso ya kidini, ikisisitiza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa operesheni ya pamoja kati ya Abuja na Washington dhidi ya magaidi, bila kulenga dini yoyote. Jeshi la Marekani pia lilieleza kuwa lilifanya shambulizi hilo kwa ombi la serikali ya Nigeria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Yusuf Tuggar, amesema operesheni hiyo bado inaendelea na akasisitiza kuwa ni juhudi ya pamoja inayotegemea taarifa za kijasusi za Nigeria, akiongeza kuwa magaidi wameua Waislamu na Wakristo kwa pamoja.
Kauli hizi zimekuja baada ya Trump kuyataja mashambulizi hayo ya anga kama “zawadi ya Krismasi” kwa Daesh, akisema yalipangwa makusudi kwa athari ya kisaikolojia.
CHANZO: TRT Afrika














