Ubalozi wa Uturuki nchini Libya umeeleza masikitiko makubwa kufuatia kifo cha Mkuu wa Jeshi la Libya, Mohammed al-Haddad, aliyepoteza maisha katika ajali ya ndege akiwa safarini kurejea kutoka ziara rasmi nchini Uturuki, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa kijeshi.
Kwa mujibu wa taarifa, viongozi kadhaa wa juu wa jeshi walikuwa miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo, akiwemo afisa mkuu wa majeshi ya nchi kavu, mkuu wa taasisi ya utengenezaji wa vifaa vya kijeshi, mshauri wa mkuu wa jeshi pamoja na mfanyakazi wa kitengo cha habari cha jeshi.
Katika ujumbe wake wa pole, ubalozi wa Uturuki ulieleza kuwa umepokea kwa huzuni kubwa taarifa za vifo hivyo, na ukatoa rambirambi kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wananchi wa Libya, familia za marehemu na wanajeshi wenzao.
Ubalozi huo pia uliomba dua kwa waliopoteza maisha na subira kwa ndugu na jamaa zao katika kipindi hiki kigumu.
Kwa upande mwingine, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki ilithibitisha kuwa mabaki ya ndege binafsi aina ya Falcon 50 yaligunduliwa na vikosi vya usalama katika wilaya ya Haymana, karibu na mji wa Ankara.
CHANZO: TRT Afrika














