Afrika

DAWASA yaanza kuchimba visima 14 kukabiliana na uhaba wa maji Dar es Salaam

DAWASA imeanza utekelezaji wa mpango wa kuchimba visima 14 jijini Dar es Salaam ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Newstimehub

Newstimehub

22 Desemba, 2025

4b2591b5a680220acaa2ded521f97b568d0ac168046b5b1f24f87b3643fb1a12

Baada ya wiki kadhaa za uhaba wa maji uliokumba maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza mpango wa kuchimba visima 14 ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa jiji hilo.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelekezo ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akilenga kupunguza adha wanayokumbana nayo wananchi ambao wamelazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya uchimbaji wa visima katika Jimbo la Kivule, Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, alisema kuwa visima vitano vitachimbwa katika Jimbo la Ilala, huku visima tisa vikitekelezwa katika Jimbo la Kivule ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, maeneo yatakayochimbwa visima katika Jimbo la Kivule ni pamoja na Kivule, Magole A, Kerezange, Bombambili na Msongola katika Mtaa wa Kidole. Aliongeza kuwa mamlaka hiyo pia inaendelea kufufua visima vya zamani katika maeneo ya Mwananyamala, Tandale na Mburahati.

Kwa sasa, DAWASA imesema kuwa visima 14 vilivyofufuliwa tayari vinafanya kazi na kutoa huduma ya maji kwa wananchi, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam.

CHANZO: TRT Afrika