Waangalizi wa Umoja wa Afrika wamesema uchaguzi uliofanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati umeendeshwa kwa amani kwa ujumla, licha ya changamoto chache za kiusalama katika baadhi ya maeneo. Uchaguzi huo ulimshirikisha Rais aliye madarakani Faustin-Archange Touadera, ambaye anawania muhula wa tatu wa uongozi.
Touadera, mwenye umri wa miaka 68, aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho akiwa katika nafasi nzuri kufuatia kuidhinishwa kwa katiba mpya mwaka 2023, iliyomruhusu kugombea tena. Uchaguzi huo ulihusisha pia wabunge pamoja na viongozi wa serikali za mitaa na mikoa, na ulifanyika kwa wakati mmoja.
Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa AU, Bernard Makuza, alisema hali ya usalama nchini iliruhusu zoezi la upigaji kura kufanyika kwa utulivu katika maeneo mengi ya nchi. Alieleza kuwa taarifa kutoka ndani ya nchi zinaonyesha kuwa mchakato uliendelea kwa amani, isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Haut-Mbomou kusini-mashariki ambako bado kuna mvutano wa kiusalama.
Baadhi ya vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi huo, vikieleza wasiwasi kuhusu uwazi wa mchakato na kuitaka serikali kufanya mazungumzo ya kisiasa. Hata hivyo, Umoja wa Afrika uliutaja uchaguzi huo kama hatua muhimu kuelekea kuimarisha demokrasia nchini humo.
Waangalizi wa AU walifuatilia zoezi hilo katika maeneo machache kati ya mikoa 20 ya nchi, na wanatarajiwa kuwasilisha ripoti yao kamili kwa serikali ndani ya mwezi mmoja. Matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa Januari 5, huku matokeo ya mwisho yakitangazwa na Mahakama ya Katiba Januari 20.
CHANZO: TRT Afrika














