Timu za utafutaji na uokoaji za Uturuki zimeongeza kasi ya shughuli zao Jumatano katika eneo la ajali ya ndege iliyosababisha kifo cha Mkuu wa Jeshi la Libya pamoja na maafisa wengine waandamizi, baada ya hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa na ukungu kuathiri operesheni usiku uliotangulia.
Ndege hiyo, iliyokuwa imembeba Mkuu wa Majeshi ya Libya Mohammed al-Haddad na ujumbe wake, ilianguka Jumanne muda mfupi baada ya kuondoka mjini Ankara, na kuua watu wote waliokuwa ndani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki alithibitisha kuwa mabaki ya ndege ya biashara aina ya Falcon 50 yaligunduliwa na vikosi vya usalama takribani kilomita mbili kusini mwa kijiji cha Kesikkavak, katika wilaya ya Haymana.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, ndege hiyo iliripoti kurejea uwanjani majira ya saa 20:32 kutokana na hitilafu ya kiufundi, kabla ya mawasiliano kukatika takribani dakika 20 baadaye.
Shughuli za uchunguzi ziliongezwa kuanzia alfajiri, huku eneo la ajali likilindwa kikamilifu na raia kuzuiwa kukaribia eneo hilo.
Mamlaka zilisema kuwa kituo maalumu cha mawasiliano na uratibu wa uchunguzi kimeanzishwa katika eneo la tukio ili kusimamia operesheni. Jumla ya wahudumu 408, pamoja na ndege saba na droni zisizo na rubani, wamehusishwa katika zoezi hilo.
Kutokana na mazingira magumu ya eneo hilo, yakiwemo matope, magari maalumu kama ambulensi zenye uwezo wa kuvuka maeneo magumu yalitumwa kusaidia operesheni.
Kufuatia tukio hilo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuomboleza vifo vya mkuu huyo wa jeshi na maafisa waliokuwa pamoja naye.
CHANZO: TRT Afrika














