Jeshi la Ethiopia limetangaza kuwa wapiganaji zaidi ya 200 wameamua kuacha mapambano na kujisalimisha kwa vikosi vya serikali katika eneo la Oromia Magharibi, hatua inayoashiria maendeleo mapya katika juhudi za kurejesha amani katika mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi iliyotolewa Jumapili, wanamgambo hao walikuwa wakifanya shughuli zao katika Wilaya ya Wollega Mashariki na walikabidhi silaha zao baada ya kufanyika kwa mazungumzo kati yao, viongozi wa eneo hilo na maafisa wa usalama. Jeshi limesema tukio hilo limetokana na muendelezo wa operesheni za kiusalama pamoja na juhudi za mazungumzo ya muda mrefu.
Eneo la Oromia Magharibi limekuwa likikumbwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya majeshi ya serikali na Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA), kundi lililojitenga baada ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018. OLA imekuwa ikidai kuwa mapambano yake yanachochewa na kile inachokitaja kama kubaguliwa na kupuuzwa kwa jamii ya Oromo, ambayo ni kubwa zaidi nchini Ethiopia.
Ingawa mamlaka zimekuwa zikitangaza matukio ya kujisalimisha au wanamgambo kukimbilia upande wa serikali mara kwa mara, ghasia bado zinaendelea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo. Aidha, ni vigumu kuthibitisha kwa uhuru ukubwa na athari za matukio hayo kutokana na vikwazo vya upatikanaji wa taarifa na kuzimwa kwa mawasiliano katika maeneo yenye migogoro. Hadi sasa, OLA haijatoa tamko lolote kuhusiana na taarifa hiyo.
CHANZO: TRT Afrika














