Watu saba, wakiwemo raia wanne wa Uholanzi, wamepatikana wakiwa hai, saa 27 baada ya ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Bandari ya Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma nchini Tanzania, kuelekea Malawi kupata ajali katika Ziwa Nyasa.
Ajali hiyo, inaripotiwa kutokea Julai 26, 2026 majira ya saa 4 asubuhi baada ya boti hiyo kupata hitilafu ya injini kisha kujaa maji kufuatia dhoruba kali na kupinduka.
Manusura hao walikaa majini kwa takribani saa 27 kabla ya kuokolewa salama majira ya saa 10 jioni ya Julai 27, 2026.
Akizungumza baada ya zoezi la uokoaji kukamilika, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Nyasa kwa ushirikiano waliouonesha katika shughuli za uokoaji.
Hali kadhalia, amewataka watumiaji wa vyombo vya usafiri ndani ya ziwa hilo, kuzingatia tahadhari na kuepuka kusafiri ziwani wakati hali ya hewa si salama.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, manusura wote saba wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri. Tukio hilo linahusisha manusura saba, wanne wao wakiwa raia wa Uholanzi.

















