Michezo

Kocha wa Korea Kusini ahojiwa bungeni baada ya matokeo mabovu Kombe la Dunia

Hong Myung-bo aliomba radhi kwa kushindwa kwa Korea Kusini kufuzu hatua ya timu 32 bora katika Kombe la Dunia lililofanyika Mexico, Marekani na Canada.

Newstimehub

Newstimehub

30 Julai, 2026

76d35862 eca2 48bd 9e8d 9952972d5d78 1785403015045

Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Korea Kusini, Hong Myung-bo, amesema kuwa, atawajibika kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo, wakati wa michuano ya Kombe la Dunia 2026.

Hong alijiuzulu baada ya timu hiyo kutolewa kwenye hatua za makundi, hali iliyopelekea kujiuzulu kwake, kabla ya kuitwa mbele ya Kamati ya Bunge inayoshughulikia Michezo na Utamaduni kujibu maswali kuhusu uchunguzi unaofanywa dhidi ya Shirikisho la Soka nchini Korea (KFA)

Hong, ambaye zamani alikuwa beki wa timu ya taifa ya Korea Kusini na aliichezea nchi hiyo katika Kombe la Dunia la mwaka 2002 lililofanyika nyumbani, amekosolewa vikali na mashabiki, wachambuzi wa soka na wanasiasa tangu timu yake ilipoondolewa baada ya kufungwa 1-0 na Afrika Kusini.

Aliporejea nchini, Hong alipokelewa kwa kuzomewa na mashabiki waliokerwa na uamuzi wake wa kumweka nahodha mkongwe Son Heung-min benchi katika mechi dhidi ya Afrika Kusini. Korea Kusini ilihitaji sare pekee ili kufuzu hatua ya mtoano.

Rais wa Korea Kusini, Lee Jae Myung alilaumu kushindwa huko kwa kile alichokiita kupandishwa madarakani kwa watu wasio na uwezo. Katika taarifa yake, hakumtaja Hong kwa jina, lakini alidokeza kuwa upendeleo na makundi ya kisiasa yaliathiri mchakato wa uteuzi wa viongozi wa juu wa soka nchini humo.

Hong mwenye umri wa miaka 57 alihojiwa kuhusu madai kwamba aliteuliwa kuingoza Korea Kusini mwaka 2024, kwa upendeleo.

Kulingana na madai hayo maafisa wa KFA walifika hadi eneo analoishi kufanya mahojiano yasiyo wazi ya kumpa wadhifa huo.

Akijibu, Hong alisema anaamini taratibu zote zilifuatwa ipasavyo na akakanusha kuwahi kuomba upendeleo au manufaa yoyote maalumu.

Wabunge pia waliibua madai kuwa alikuwa akilipwa mshahara wa takriban Dola milioni 2.6 za Marekani, kiwango kinachodaiwa kuwa miongoni mwa mishahara mikubwa kwa makocha wa timu za taifa. Hong amekanusha madai hayo, lakini alikataa kutaja kiwango halisi cha mshahara wake.

Pia aliomba radhi kwa kushindwa kwa Korea Kusini kufuzu hatua ya timu 32 bora katika Kombe la Dunia lililofanyika Mexico, Marekani na Canada.

“Nilikuwa kocha mkuu, na nafasi hiyo huhukumiwa kwa matokeo. Kwa kuwa hatukufanya vizuri katika Kombe hili la Dunia, nachukua jukumu kamili kwa kila kilichotokea,” amesema.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini vilikuwa vimeitaja timu ya mwaka 2026 kuwa “kizazi cha dhahabu”, huku matarajio makubwa yakiwekwa kwa kikosi kilichokuwa na nyota kama Son Heung-min, beki wa Bayern Munich Kim Min-jae, na kiungo wa zamani wa Paris Saint-Germain Lee Kang-in.