Polisi nchini Afrika Kusini walisema siku ya Jumatatu kuwa wamewakamata watu watatu kuhusiana na mauaji ya wanawake katika eneo moja viungani mwa jiji la Johannesburg.
Mauaji ya wanawake tisa walio kati ya umri wa miaka ishirini na thelathini yamefanyika katika manispaa ya Ekurhuleni kwa takriban kipindi cha zaidi ya miezi miwili na kusababisha hasira kote nchini Afrika Kusini.
Polisi wamekuwa wakichunguza mauaji yanayohusiana na hayo, kuzua hofu kuwa kuna muuaji au wauaji wanaotekeleza msururu wa mauaji katika eneo hilo.
Washukwia hao, wanawake wawili na mwanamume mmoja, walitarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu baada ya kukamatwa kuhusiana na mauaji ya mwanamke ambaye mwili wake ulipatikana wiki iliopita eneo la Ekurhuleni, mashariki mwa jiji la Johannesburg.
Uchunguzi unaendelea
Hata hivyo, uchunguzi haujahusisha mauaji hayo na yale ya wanawake wanane wengine wanane.
Mamlaka zinasema kuwa haifahamiki wazi kama mauaji yote yanahusiana na mauaji mengine, ingawa walisema wametambua kuwa na uhusiano katika baadhi ya mauaji na kutoa tahadhari kwa wanawake eneo la Ekurhuleni kuwa makini.
Waziri wa Masuala ya Polisi Firoz Cachalia alisema siku ya Jumapili kuwa kufikia sasa hakuna ushahidi kamili kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na muuaji anayelenga watu mahsusi, “lakini uchunguzi bado unaendelea kubaini zaidi.”

















