Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza mabadiliko makubwa katika ratiba ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), likisema kuwa mashindano hayo yataanza kuandaliwa kila baada ya miaka minne kuanzia toleo la mwaka 2028. Awali, AFCON ilikuwa ikifanyika kila baada ya miaka miwili.
Akizungumza Jumamosi, Rais wa CAF Patrice Motsepe alisema uamuzi huo ni sehemu ya mageuzi mapana yanayolenga kulifanya soka la Afrika liendane vizuri zaidi na kalenda ya kimataifa, ambayo kwa sasa ina mashindano mengi yanayokinzana.
Motsepe alieleza kuwa licha ya AFCON ya kila baada ya miaka miwili kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa vyama vya soka barani Afrika, pengo hilo litazibwa na kuanzishwa kwa Ligi ya Mataifa ya Afrika, itakayokuwa ikichezwa kila mwaka, sawa na Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League).
Akizungumza mjini Rabat, Morocco, alisema AFCON ijayo itafanyika mwaka 2027 nchini Tanzania, Kenya na Uganda, huku toleo litakalofuata likipangwa kufanyika mwaka 2028. CAF pia itafungua mchakato wa nchi kuwasilisha maombi ya kuwa wenyeji wa mashindano ya mwaka 2028.
Kwa mujibu wa Motsepe, baada ya Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA mwaka 2029, CAF itaendesha Ligi ya Mataifa ya Afrika yenye zawadi kubwa zaidi za fedha, rasilimali zaidi na ushindani wa juu.
Kwa muda mrefu, AFCON imekuwa ikikumbwa na changamoto za ratiba kutokana na msongamano wa kalenda ya kimataifa, hali iliyosababisha mashindano hayo kuhamishwa mara kadhaa kati ya Januari, Februari, Juni na Julai. Mabadiliko hayo yalilazimishwa pia na masuala ya hali ya hewa, michuano ya FIFA na mashindano ya vilabu barani Ulaya.
Motsepe alisema mageuzi hayo yanalenga kuleta uwiano bora kati ya maslahi ya soka la Afrika na wachezaji wa Kiafrika wanaocheza katika vilabu vikubwa Ulaya, ili waweze kushiriki kikamilifu mashindano ya bara lao.
Aidha, CAF imetangaza kuwa zawadi ya fedha kwa mshindi wa AFCON itakayofanyika Morocco itaongezwa hadi dola za Marekani milioni 10, kutoka dola milioni saba zilizotolewa kwa mshindi wa toleo la 2024 nchini Ivory Coast.
CHANZO: TRT Afrika














