Chama cha upinzani nchini Uganda, People’s Front for Freedom, kimetangaza kuwa afya ya mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye, anayezuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala, imezorota na inaendelea kudhoofika. Besigye alipelekwa usiku katika kituo cha afya mjini Kampala, jambo lililozua hofu miongoni mwa wafuasi wake.
Chama chake kimetaka apewe nafasi ya kukaguliwa na madaktari wake binafsi pamoja na familia yake, kikisisitiza kuwa serikali na mamlaka za magereza zinapaswa kuwajibika kikamilifu kwa afya yake. Besigye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, ambayo anadai ni ya kisiasa.
Hata hivyo, msemaji wa Idara ya Magereza, Frank Baine, amekanusha madai ya kudhoofika kwa afya ya Besigye, akisema kuwa kilichofanyika ni ukaguzi wa kawaida na kwamba asubuhi yake aliendelea na mazoezi kama kawaida.
Besigye, aliyewahi kuwa kiongozi maarufu wa upinzani kabla ya kupanda kwa umaarufu wa Bobi Wine, aligombea urais mara ya mwisho mwaka 2016. Uganda kwa sasa iko katika mzozo wa kisiasa baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi wa uchaguzi kwa kura 71.6%, huku Bobi Wine akipata 24.7% na kukataa matokeo hayo akiyataja kuwa ya kighushi.
CHANZO: TRT Afrika














