Mahakama nchini Madagascar imeamuru kuwekwa kizuizini kwa wanasiasa wawili wa karibu na aliyekuwa Rais Andry Rajoelina, wakikabiliwa na mashtaka ya kuhatarisha usalama wa taifa. Ni kuhusu Marie Michelle Sahondrarimalala, mbunge wa zamani na aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu, pamoja na Richard Ravalomanana, aliyekuwa Rais wa Seneti na Jenerali mstaafu.
Sahondrarimalala alikamatwa baada ya nyumba yake kupigwa msako na kuhojiwa na polisi wa kiuchumi, kisha kupelekwa mbele ya Parquet ya Mahakama Kuu na hatimaye kupelekwa gerezani Avaradrano. Wakati huo huo, Ravalomanana, aliyekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Desemba, alihamishiwa gereza la Imerintsiatosika baada ya kuhojiwa na Parquet ya Anosy.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri Narindra Rakotoniaina, watu wengine 12 wamewekwa chini ya uangalizi wa mahakama kwa tuhuma za kushirikiana katika mpango wa kugawa fedha kwa lengo la kudestabilisha hali ya kisiasa. Ravalomanana pia anakabiliwa na mashtaka ya ushirikiano katika mauaji na majeraha ya makusudi, kutokana na tuhuma za kuhusika katika mashambulizi dhidi ya waandamanaji wa Gen Z.
Hali hii inajiri wakati Madagascar ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa ulioanza Septemba 25, uliosababisha kuondolewa kwa Rajoelina madarakani na kupelekea kuibuka kwa Colonel Michaël Randrianirina kama Rais wa Jamhuri ya Refondation.
CHANZO: AA














