Beki wa Hispania, Marc Cucurella, alionesha tattoo mpya ya kocha Luis de la Fuente kwenye mkono wake wa kushoto siku ya Jumanne, akitimiza ahadi aliyoiweka kabla ya Hispania kushinda Kombe la Dunia.
Beki huyo wa kushoto aliapa kwamba angechora tattoo yenye sura ya kocha huyo endapo Hispania ingeshinda michuano hiyo.
Ahadi hiyo ilitimia baada ya Hispania kuifunga Argentina kwa bao 1-0 katika fainali iliyochezwa New Jersey, Julai 19.
Mlinzi huyo wa kushoto, aliyehamia Real Madrid akitokea Chelsea, alionesha tattoo yake mpya mitandaoni, ikiwa na maneno: “Ahadi imetimizwa.”
Katika tattoo hiyo, De la Fuente anaonekana akiwa amevalia suti na akiwa ameshikilia Kombe la Dunia, ambalo ni la pili kwa Hispania baada ya mara ya kwanza kutwaa ubingwa huo mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Cucurella, mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na Real Madrid akitokea Chelsea kabla ya mchezo wa kwanza wa Hispania kwenye Kombe la Dunia, ambao uliisha kwa sare ya 0-0 dhidi ya Cape Verde. De la Fuente alisema matokeo hayo ya kukatisha tamaa yaliisaidia timu kupata motisha zaidi katika safari yao ya kutwaa ubingwa.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliteuliwa kuwa mrithi wa Luis Enrique mwaka 2022, na pia ameiongoza ‘La Roja’ kutwaa ubingwa wa Euro 2024 pamoja na Ligi ya Mataifa (Nations League) mwaka 2023.

















