Serikali ya Israel imeanza mchakato wa kufuta vibali vya mashirika ya kimataifa ya misaada yanayofanya kazi katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikidai kuwa baadhi yao hayajatimiza masharti mapya ya usajili na usalama.
Kwa mujibu wa mamlaka za Israel, mashirika 37 yapo kwenye orodha ya yale yanayokusudiwa kufutiwa leseni, yakiwemo mashirika maarufu kama Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) na ActionAid. Serikali inadai kuwa baadhi ya mashirika hayo yameshindwa kuwasilisha taarifa kamili za wafanyakazi wao, hasa Wapalestina, kwa madhumuni ya uchunguzi wa kiusalama.
Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zinaeleza kuwa zaidi ya mashirika 12 tayari yamepokea taarifa rasmi yakielezwa kuwa vibali vyao vitafutwa kuanzia Januari mosi, huku yakitakiwa kusitisha kabisa shughuli zao ifikapo Machi mosi. Mamlaka zimedai kuwa baadhi ya mashirika yalikataa kutoa orodha kamili za wafanyakazi wao, hatua iliyotajwa kukiuka taratibu mpya.
Hatua hiyo inasimamiwa na timu ya mawaziri chini ya Wizara ya Masuala ya Diaspora na Kupambana na Chuki dhidi ya Wayahudi, ambayo imesisitiza kuwa mashirika lazima yachague kati ya kuzingatia masharti mapya au kuondoka katika maeneo hayo.
Wachambuzi na vyombo vya habari vimeonya kuwa uamuzi huo unaweza kuhatarisha uwepo wa muda mrefu wa mashirika ya misaada ya kimataifa ambayo yamekuwa yakitoa huduma muhimu kwa wakazi wa Gaza na Ukingo wa Magharibi kwa miongo kadhaa. Hatua hii pia inakuja kufuatia hatua za awali za Israel dhidi ya UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina.
CHANZO: TRT Afrika














