Afrika

Taasisi ya Thabo Mbeki yakosoa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania

Taarifa hiyo inakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuzindua tume itakayochunguza vurugu zilizotokea siku na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, huku akiipa tume hiyo siku 90 za kufanya uchunguzi huo.

Newstimehub

Newstimehub

24 Novemba, 2025

1a4408c972d621745c4146b3b57fa21283c1d3c721d8a6ae0ef962fc2b62f4b3

Taasisi ya Thabo Mbeki ya nchini Afrika Kusini imekosoa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Katika taarifa yake iliyotolewa Novemba 23, 2025, taasisi hiyo imesema kuwa, imesikitishwa na uvunjifu wa amani uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu nchini humo, ikisema kuwa imekosa ‘serikali halali’.

Taasisi hiyo, ambayo imepewa jina la rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, imesisitiza kuwepo na mjadala wa kitaifa wenye uwazi na ukweli ili kutatua hali ya sasa nchini Tanzania.

Kulingana na taasisi ya Thabo Mbeki, matokeo ya urais na ubunge nchini Tanzania, hayaakisi matakwa ya Watanzania wenyewe.

“Wakati baadhi ya Watanzania wakisema kuwa ni wakati muafaka kwa maridhiano, tunaamini kuwa suluhisho pekee ni mjadala wa kitaifa wenye uwazi na ukweli,” ilisomeka taarifa hiyo iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Thabo Mbeki, Max Boqwana.

Kulingana na taasisi hiyo, hilo ndilo suluhisho pekee la kuirudishia Tanzania, sifa yake ya kuwa kinara wa amani na utulivu barani Afrika.

Taarifa hiyo inakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuzindua tume itakayochunguza vurugu zilizotokea siku na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, huku akiipa tume hiyo siku 90 za kufanya uchunguzi huo.

Rais Samia aliyerejea madarakani kwa takribani asilimia 98 ya kura, ametaja baadhi ya majukumu ya tume hiyo inayoongozwa na majaji wakuu wastaafu kuwa ni kuangalia sababu iliyoleta kadhia hiyo, kiini cha tatizo na madai ya vijana walioingia barabarani kudai haki.