Sudan Kusini inakabiliwa na changamoto ya mapato huku jirani yake Sudan akiamua kufunga kituo kikuu cha mafuta.
Wizara ya Nishati na Petroli ya Sudan imeamuru kufungwa kwa dharura kwa vituo vya mafuta katika eneo la Heglig karibu na mpaka na Sudan Kusini kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani mapema Jumamosi.
Shambulio hilo, lililolaumiwa kwa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), lililenga Kambi ya Operesheni ya Heglig karibu saa mbili na nusu asubuhi, na kuharibu kituo cha uwanja wa ndege na kusababisha kuhamishwa kwa wafanyakazi, kulingana na barua ya Wizara ya Agosti 30.
Uwanja wa ndege haujafanya kazi tangu Aprili 2023.
Uamuzi wa serikali ya Sudan kama ilivyoelezwa katika barua yake, unafuatia sababu za kiusalama ikiwemo mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanayohusishwa na Vikosi vya Rapid Support Forces, RSF.
Vikosi vya serikali vimekuwa vikipambana na RSF tangu Aprili 2023.
Hii si habari njema kwa jirani yake Sudan Kusini ambayo kwa asilimia kubwa, inategemea miundombinu ya Sudan katika uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia Bahari Nyekundu.
Kituo cha mafuta cha Heglig kinachofungwa kiko kando ya mpaka kusini mwa Sudan na ni kituo kikuu cha usindikaji wa mafuta ya Sudan Kusini. Uzalishaji wa mafuta ni tegemeo kuu la mapato kwa Sudan Kusini.














