Mkuu wa ujasusi wa Uturuki, Ibrahim Kalin, amekutana na ujumbe wa Hamas mjini Istanbul, akiwemo Khalil al-Hayya, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya kundi hilo na kiongozi wa timu ya mazungumzo. Mazungumzo hayo yalihusu makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, ambayo sasa yameingia katika awamu ya pili.
Pande hizo mbili zilikubaliana kushirikiana katika kuongeza misaada ya kibinadamu, kufungua Kivuko cha Rafah, kuanzisha Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Gaza, na kushughulikia masuala mengine yanayohusiana na hali ya eneo hilo.
Ujumbe wa Hamas ulitoa shukrani kwa Rais Recep Tayyip Erdoğan kwa jukumu la Uturuki katika usuluhishi na dhamana ya amani, wakisisitiza nafasi ya Ankara katika awamu ya pili ya mpango wa Gaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, tangu Oktoba 2023 Israel imewaua zaidi ya watu 71,000 na kujeruhi zaidi ya 171,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Licha ya kutangazwa kwa kusitisha mapigano Oktoba 10, mashambulio yameendelea, na kusababisha vifo vya Wapalestina 481 na majeruhi 1,313.
CHANZO: TRT Afrika














