Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa limefanikiwa kumuua kamanda wa Boko Haram, Abu Khalid, pamoja na wapiganaji wengine 10 katika operesheni iliyofanyika msituni Sambisa, jimbo la Borno. Abu Khalid alitajwa kuwa wa pili kwa uongozi wa kundi hilo na alikuwa na jukumu kubwa la kuratibu mashambulizi na mipango ya kigaidi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, hakuna askari wa Nigeria aliyeuawa katika operesheni hiyo, na juhudi za kupambana na ugaidi zinaendelea katika misitu ya kaskazini mashariki mwa nchi.
Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, na tangu 2009 maelfu ya watu wamepoteza maisha. Kuanzia 2015, kundi hilo limepanua mashambulizi yake hadi Cameroon, Chad na Niger, na kuua zaidi ya watu 2,000 katika eneo la Ziwa Chad. Mashambulizi haya yamesababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao.
CHANZO: TRT Afrika














