Maelfu ya wakazi wa Istanbul wamejitokeza katika maandamano makubwa ya kuunga mkono Wapalestina, wakitoa wito wa kusitishwa kwa vita na kumalizwa kwa mateso yanayoendelea Gaza. Maandamano hayo yalibeba ujumbe wa umoja, haki na mshikamano wa kimataifa.
Chini ya kaulimbiu “Hatuwezi Kunyamaza, Hatuwezi Kusahau Palestina”, maandamano hayo yaliandaliwa na jukwaa la muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali, yakihusisha zaidi ya asasi 400 za kiraia na kidini. Siku ilianza kwa swala ya Alfajiri katika miskiti mikuu ya kihistoria ikiwemo Ayasofya, Sultanahmet na Suleymaniye, kabla ya waandamanaji kuelekea Daraja la Galata.
Washiriki walibeba bendera za Uturuki na Palestina, wakivaa keffiyeh na kupaza sauti za kudai uhuru wa Palestina. Viongozi wa asasi za kiraia na kidini walihutubia umati huo, wakisisitiza umuhimu wa mshikamano wa wananchi na matumaini ya amani na haki kwa watu wa Palestina na mji wa Jerusalem.
Maandamano hayo yalifanyika kwa amani chini ya ulinzi mkali wa polisi, huku waandamanaji wakituma ujumbe mzito wa mshikamano kutoka Istanbul kwenda kwa jumuiya ya kimataifa, wakieleza matumaini kuwa mwaka 2026 utaleta haki, amani na mwisho wa mateso Gaza.
CHANZO: TRT Afrika














