Hatua ya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro pamoja na mkewe imeibua mjadala na wasiwasi mkubwa duniani, huku Rais Donald Trump akisifia operesheni hiyo lakini jumuiya ya kimataifa ikiitazama kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Rais Trump alisema shambulio la kushtukiza lililofanyika usiku wa manane Jumamosi, lililofahamika kama operesheni “Absolute Resolve”, lilitekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kuonyesha uwezo wa kijeshi wa Marekani. Maduro na mkewe Cilia Flores walipelekwa Marekani ambako wamefunguliwa mashtaka mbalimbali, yakiwemo ya ulanguzi wa dawa za kulevya na makosa ya silaha.
Hata hivyo, serikali ya Venezuela imekanusha madai ya Washington, ikitaja tukio hilo kama utekaji nyara. Makamu wa Rais Delcy Rodríguez, anayekaimu urais kwa baraka za Mahakama Kuu ya nchi hiyo, amesema Maduro bado ndiye rais halali wa Venezuela na kwamba Marekani imeingilia uhuru wa taifa hilo.
Kimataifa, hatua ya Marekani imekabiliwa na shutuma kali. Urusi na China zililaani shambulio hilo na kutangaza utayari wao wa kushirikiana na watu wa Venezuela. Nchi kadhaa za Amerika Kusini pamoja na Uhispania zimeonya kuhusu athari za operesheni hiyo kwa usalama na utulivu wa kikanda.
Afrika Kusini, Iran na Ufaransa nazo zimeshutumu vikali shambulio hilo, huku Umoja wa Afrika ukilaani uvamizi huo. Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake na kutoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa, bila kutoa lawama ya moja kwa moja.
Licha ya upinzani huo, Rais Trump ameendelea kutoa vitisho vya kuchukua hatua zaidi dhidi ya Venezuela, akionya pia kuwa anaweza kulenga nchi nyingine za eneo hilo, hatua inayozidi kuongeza hofu ya kuenea kwa mgogoro wa kikanda.
CHANZO: TRT Afrika














