Liverpool imepiga hatua muhimu kuelekea kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kuichapa Crystal Palace mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyochezwa Anfield.
Alexander Isak aliifungia Liverpool bao la kwanza kabla ya Andy Robertson kuongeza la pili muda mfupi baadaye katika kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, wasiwasi mkubwa umetanda kwa mashabiki wa Liverpool baada ya nyota wao Mohamed Salah kutolewa uwanjani katika kipindi cha pili akiwa na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja.
Crystal Palace walipunguza pengo kupitia Daniel Munoz, lakini Florian Wirtz alifunga bao la tatu dakika za nyongeza na kuhakikisha Liverpool inachukua pointi zote tatu.
Matokeo hayo yanaiweka Liverpool nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na kuipa pengo la pointi nane dhidi ya Brighton walio nafasi ya sita.














