Wachimba migodi haramu kumi na nne wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa vibaya baada ya mgodi kutitia nchini Afrika Kusini, polisi walisema siku ya Jumanne.
Hakukuwa na taarifa kamili kuhusu wachimba migodi hao, ikiwemo uraia wao, huku maafisa wakielekea eneo la tukio, msemaji wa polisi wa mkoa Kanali Adele Myburgh ameiambia AFP.
“Wachimba migodi kumi na nne wameuawa katika mgodi ambao ulikuwa hautumiki,” taarifa ya polisi ilisema. Wachimba migodi wengine wanane walijeruhiwa vibaya, Myburgh aliiambia AFP.
Janga hilo lilitokea karibu na mji wa Rustenburg, karibu kilomita 100 kaskazini magharibi mwa jiji wa Johannesburg.
Wachimba migodi haramu
Maelfu ya wachimba migodi ambao hawajasajiliwa wanaojulikana kama “zama zama” wako nchini Afrika Kusini, wakivamia migodi iliyoachwa kwa ajili ya kutafuta dhahabu na madini mengine mara nyingi katika mazingira hatarishi.
Wanakuja kutoka Kusini mwa Afrika, kutokana na umaskini na ukosefu wa ajira, na sekta hiyo imehusishwa na uhalifu wa magenge, mauaji, madai ya kikombozi na shughuli zingine zisizo halali.
“Maeneo wanayofanya kazi hayako salama. Kwa hiyo ni moja ya yale maeneo ambapo mgodi umetitia,” Myburgh alisema.
“Wanaingia kwenye migodi ambayo imeachwa … hakuna miundombinu, hakuna usalama,” alisema.

















