Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) imetambua visima tisa vinavyoweza kuwa na mafuta katika eneo la Kasuruban, vinavyodaiwa kuwa na “hifadhi mpya kubwa za mafuta ghafi,” ilisema Jumanne.
Ugunduzi huo unaweza kuongeza rasilimali za mafuta ghafi katika hifadhi la bonde la Albertine, ambapo makampuni ya Ufaransa na ya China tayari yanaendesha machimbo ya mafuta yanayotarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara katika nusu ya pili ya mwaka ujao.
UNOC ilipata hifadhi Kasuruban yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,285 mwaka 2023 baada ya kusaini mkataba wa kugawana uzalishaji (PSA) na serikali.
Taarifa ya UNOC kwenye mtandao wa kijamii X iliongeza kwamba makadirio ya awali yalionyesha visima hivyo tisa vilivyotambuliwa vinaweza kutoa bareli milioni 600 za mafuta ghafi yanayoweza kuchimbwa. Haikufafanua lini ugunduzi ulifanywa wala kutoa maelezo zaidi.
Hivi sasa, akiba ya mafuta ya Uganda iliyothibitishwa kuwa yanaweza kuchimbwa iko bareli bilioni 1.65.














