Takriban watu 21 wamefariki dunia na wengine 32 kujeruhiwa kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika mkoa wa Safi, kusini mwa mji mkuu Rabat, mamlaka za Morocco zimesema. Mafuriko hayo yalitokea baada ya mvua kubwa kunyesha kwa muda mfupi lakini kwa kiwango kikubwa, na kusababisha uharibifu wa nyumba, maduka, barabara na kusomba magari katika mji mkongwe wa Safi.
Tukio hilo linajiri wakati Morocco ikishuhudia hali ya hewa kali, ikiwemo mvua kubwa na theluji katika Milima ya Atlas, baada ya nchi hiyo kukabiliwa na ukame wa muda mrefu uliodumu kwa takriban miaka saba. Mamlaka zimesema juhudi za uokoaji na tathmini ya uharibifu zinaendelea.
CHANZO: TRT Afrika














