Marekani itaanza hatua za kuondoa pole pole msaada wake wa kifedha kwa mpango wa kukabiliana na VVU nchini Namibia, ikiwa ni miongoni mwa nchi za kusini mwa Afrika zinazohisi athari za kuondolewa kwa misaada ya kigeni na utawala wa Marekani.
Marekani itaipatia Namibia Dola milioni 45 kwa ajili ya mpango wake wa kukabiliana na HIV katika mwaka wa fedha wa 2027, lakini nchi hiyo baadae itaanza kufadhili programu zake za VVU yenyewe, huku Marekani ikitoa tu “ushirikiano wa kiufundi,” kama pande zote mbili zilivyoeleza katika taarifa.
Namibia imepokea karibu Dola milioni 45 kila mwaka kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani kwa Ustawi wa Watu wenye UKIMWI (PEPFAR) katika miaka ya hivi karibuni. Marekani inasema imechangia zaidi ya Dola bilioni 1.1 katika kuisaidia Namibia kukabiliana na VVU tangu 2003.
Ingawa kuondolewa kwa ufadhili kulitarajiwa tangu sera ya utawala wa Trump ya “Marekani Kwanza” ilipotangazwa kuhusu misaada ya kigeni, hatua hii inafuata uamuzi wa Namibia wa kukataa masharti yaliyopendekezwa ya kushirikiana taarifa za afya na sampuli za kibaolojia na Marekani. Namibia ilitaja faragha, udhibiti wa taifa na masuala ya kisheria kama sababu za uamuzi wake.
Utawala wa Trump umekuwa ukitia saini makubaliano ya nchi kwa nchi ambayo Washington inasema yataepusha utegemezi kwa wafadhili, kuongeza ufadhili wa ndani na kulinda maslahi ya Marekani. Marekani imesaini makubaliano na takriban nchi 30 tangu mwishoni mwa mwaka jana, nyingi kati yao barani Afrika.
Lakini Ghana ilikataa makubaliano yaliyopendekezwa kwa sababu ya ufikiaji wa data nyeti za afya, Zimbabwe ilijiondoa kutoka katika kifurushi cha Dola 367 milioni kwa sababu za aina hiyo, na pingamizi mahakamani imeweka makubaliano ya Kenya ya Dola 2.5 billion kusimama. Zambia pia imekuwa ikipinga mahitaji ya kushirikiana data.
Maafisa wa Namibia waliwahi kusema masharti yaliyopendekezwa kwa umbo lao la awali yalikuwa “hayajafuata sheria za kitaifa za Namibia” na yalivunja ulinzi wa faragha wa katiba pamoja na uhuru wa kitaifa juu ya rasilimali za kibaolojia.
Ripoti zinasema serikali zote mbili zinaendelea kujadili makubaliano mapya ya kiafya ya pande mbili.
Taarifa ya pamoja ilisema Namibia imezidi malengo ya UNAIDS kwa kufikia lengo la 96% ya watu wanaoishi na VVU kujua hadhi yao, 98% ya wale walioambukizwa kupata matibabu, na 98% ya waliopokea matibabu kufikia udhibiti wa virusi.

















