Utafiti mpya umebaini kuwa moshi unaotokana na moto wa misitu ya Amazon, licha ya madhara yake makubwa, unaweza pia kuchangia ukuaji wa miti katika maeneo ambayo hayajaguswa na ukataji. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Antwerp nchini Ubelgiji na kituo cha CREAF Barcelona wanasema moshi huo hubeba virutubisho, hasa fosforasi, vinavyofanya kazi kama mbolea ya asili.
Virutubisho hivyo vinapowekwa kwenye udongo wa misitu, vinachochea ukuaji wa miti na kuongeza uwezo wa misitu kufyonza hewa ya kaboni. Kwa mujibu wa utafiti, fosforasi ina athari kubwa zaidi kwa ukuaji wa miti kuliko joto au mvua. Data ya satelaiti imeonyesha viwango vya juu vya usanisinuru katika maeneo yaliyopokea fosforasi nyingi.
Kwa wastani, kila miligramu moja ya fosforasi kwa mita ya mraba huongeza hifadhi ya kaboni kwa takribani gramu 7.4 kwa mwaka. Miti pia huunda matawi yenye msongamano zaidi, jambo linalosaidia kunasa mwanga wa jua na kaboni dioksidi.
Hata hivyo, watafiti wameonya kuwa moto wa misitu unabaki kuwa tishio kubwa kwa mazingira, wakisisitiza kuwa matokeo haya yanaonyesha jinsi mifumo ya ikolojia ilivyo na uhusiano wa karibu.
CHANZO: AA














