Afrika

Waandamanaji nchini Madagascar wamtaka rais wa nchi hiyo ajiuzulu

Polisi wanatumia mabomu ya machozi, na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji.

Newstimehub

Newstimehub

10 Oktoba, 2025

8c9e44e567239f2f28b9c41070310ef2e6fce61d0cf6a80a2b5c750f799fc250

Takriban waandamanaji 1,000 waliandamana dhidi ya serikali katika mji mkuu wa Antananarivo nchini Madagascar, Alhamisi, wakimtaka Rais Andry Rajoelina ajiuzulu.

Maandamano hayo yalifanyika wakati wa machafuko makubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini Madagascar, ambapo polisi walitumia mabomu ya machozi, na risasi za mpira kutawanya umati wa waandamanaji.

Maandamano hayo, yanayoendeshwa na kizazi cha “Gen Z Madagascar,” muungano wa wanafunzi na vijana, yalichochewa na hasira kutokana na kukatika kwa huduma za maji na umeme, lakini baadaye yaligeuka kuwa maandamano ya kumtaka Rais Rajoelina ajiuzulu.

Hali hiyo ilizidi kuzorota, licha ya Rais Rajoelina kuvunja serikali yake na kuteua sura mpya katika baadhi ya wizara.

SIku ya Jumatano, Rais Rajoelina alilaumu wale waliokuwa wakimtaka ajiuzulu kwa kutaka kuharibu nchi, huku akisema mbele ya mkutano kwenye ikulu kwamba atabadilisha hali ya nchi ndani ya mwaka mmoja.

Mawakili wa waandamanaji walieleza waandishi wa habari kuwa wateja wao 28 wamepelekwa kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka rasmi.