Watu wapatao 37 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama mtoni kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Tukio hilo lilitokea Mto Luangatshimo Jumatano iliyopita, na kuja kuthibitishwa na vyombo vya habari Jumatatu.
Chombo hicho kilikuwa na abiria 42 wakati kikitokea mji wa Lovua kuelekea Nangalula, kabla hakijapoteza muelekeo katika yam to huo, kulingana na afisa wa eneo hilo, aliyejitambulisha kama Nico Ngenza Kitambala.
“Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwani kuna watu 37 ambao bado hawajulikani walipo. Timu za uokoaji zinaendelea na jitihada japo mto bado umechafuka,”alisema Kitambala.
Kulingana na Kitambala, tukio hilo lilitokana na ‘makosa ya kibinadamu’, akiongeza kuwa watu kadhaa wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Tukio hilo linakuja siku chache baada ya kadhaa kuripotiwa kupotea ndani ya Ziwa Mai-Ndombe.














