Wafanyakazi wa afya katika kituo cha matibabu ya Ebola mashariki mwa Congo wamefanya mgomo siku ya Jumamosi kufuatia tatizo la malipo, na kusababisha huduma kusita wakati ambapo nchi hiyo inakabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Idadi ya maambukizi ya Ebola yaliyothibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefikia 2,973, ikiwemo vifo 1,309, kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa Ijumaa ambapo serikali inasema ni mlipuko ulioweka rekodi ya kuenea kwa kasi.
Shughuli zote zilikwama katika Kituo cha Kutoa Matibabu ya Ebola cha Elikya kilichopo Bunia, mkoa wa Ituri, hii ni baada ya madaktari, wauguzi na walinzi kugoma kufanya kazi.
Takriban wafanyakazi wa afya mia moja waliandamana nje ya kituo siku ya Jumamosi.
Walisema kutolipwa kwa marupurupu kunakatisha tamaa na kutatiza huduma kwa wagonjwa, hivyo kuitaka serikali kulipa stahiki zao ili warudi kazini.

















