Marekani na mataifa ya Ulaya zimeitaka Rwanda na waasi wa M23 kusitisha mara moja mashambulizi mashariki mwa DRC, wakionya kuwa mapigano hayo yanatishia utulivu wa eneo lote. Katika taarifa ya pamoja, muungano huo umezitaka RDF na M23 kuacha operesheni za kijeshi na M23 kurejea kwenye makubaliano ya mazungumzo ya Qatar. Wito huu unakuja siku chache baada ya marais wa Rwanda na DRC kutia saini makubaliano mjini Washington, wakati ambapo mashambulizi mapya yameripotiwa katika maeneo ya mpakani. Marekani na EU pia zimeeleza wasiwasi juu ya ongezeko la matumizi ya ndege zisizo na rubani katika mzozo huo.
CHANZO: TRT Afrika














